Na Mwandishi Wetu
KAMISHNA wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas James Lyimo, ameipongeza Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kwa mchango wake mkubwa katika kulinda afya ya wananchi kupitia usimamizi madhubuti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa pamoja na bidhaa nyingine za afya.
Kamishna Lyimo alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TMDA katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, ambako alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo pamoja na elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya dawa na bidhaa za afya.
Katika ziara hiyo, Kamishna Lyimo alipokelewa na Meneja wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza, ambaye alimueleza kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo ya kusimamia ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na bidhaa nyingine za afya kabla ya kufikishwa kwa watumiaji.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Kamishna Lyimo alisema TMDA imeendelea kutekeleza wajibu wake kwa weledi, hatua inayochangia kuhakikisha Watanzania wanapata bidhaa za afya zilizo salama na zenye viwango vinavyokubalika.
Alisema usimamizi huo ni nguzo muhimu katika kulinda afya ya jamii na kuimarisha mapambano dhidi ya matumizi holela ya dawa pamoja na bidhaa nyingine zinazoweza kuhatarisha afya ya wananchi.
"TMDA ina jukumu kubwa katika kuhakikisha bidhaa za afya zinazowafikia wananchi zinakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi. Hili ni jambo muhimu katika kulinda afya ya Watanzania na kuzuia matumizi yasiyo sahihi ya dawa," alisema.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya TMDA na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza ufanisi katika kudhibiti matumizi mabaya ya dawa na bidhaa nyingine zinazoweza kutumika kinyume cha sheria.
Kamishna Lyimo pia aliipongeza TMDA kwa kutumia Maonesho ya Sabasaba kama jukwaa la kuwafikia wananchi wengi kwa kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa, umuhimu wa kutumia bidhaa za afya zilizosajiliwa pamoja na tahadhari dhidi ya bidhaa zisizokidhi viwango.
Alieleza kuwa elimu hiyo ni nyenzo muhimu katika kujenga jamii yenye uelewa wa masuala ya afya, kupunguza madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya dawa na kuongeza ushiriki wa wananchi katika kulinda afya zao.
Kwa upande wake, TMDA imeendelea kutumia maonesho hayo kutoa huduma na elimu kwa umma kuhusu usalama wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa zilizosajiliwa na zinazokidhi viwango vya ubora kwa ajili ya kulinda afya na ustawi wa jamii.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)

0 comentários :
Post a Comment