Kampuni inayotoa huduma za fedha kidigitali, Mixx kwa kushirikiana na kampuni ya Hisense, leo wametambulisha kampeni ya kitaifa itakayowawezesha Watanzania kujishindia zawadi mbalimbali kupitia matumizi ya huduma za Mixx.
Kampeni hiyo iliyopewa jina la ‘Jimixx FIFA World Cup 2026 na Hisense’ yenye kauli mbiu isemayo ‘Kila Muamala Ni Bao la Ushindi’ inaanza rasmi Mei hadi mwisho wa Julai 2026 ikiwa na lengo la kusheherekea Kombe la Dunia na wapenzi wa mchezo wa mpira wa miguu sambamba na kuhamasisha matumizi ya fedha kidijitali.
Kupitia kampeni hii, wateja watapata nafasi ya kujishindia fedha taslimu kiasi cha Shilingi milioni 1 kila siku, vifaa vya kisasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kutoka Hisense vikijumuisha runinga za inchi 50, spika aina ya PartyBox pamoja na friji za milango miwili. Aidha, washindi watano watajishindia safari ya kwenda Mexico kushuhudia mechi za Kombe la Dunia mubashara na kulipiwa gharama zote.
Mbali na zawadi hizo, mshindi mmoja wa droo kuu ataibuka na ushindi wa shilingi milioni 50.
Wateja watakaotumia huduma za Mixx ikiwemo Lipa Kwa Simu, kutuma fedha Mixx kwenda Mixx, kulipia bili mbalimbali kama LUKU na visimbuzi, malipo ya michezo ya kubashiri, uwekezaji kwenye soko la hisa (DSE) pamoja na miamala yote itakayofanyika kupitia Mixx Super App, wataingia moja kwa moja kwenye droo ya kampeni hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Bi. Angelica Pesha alisema kampeni hiyo ni dhamira ya Mixx kuunganisha watanzania kupitia michezo huku ikihamasisha ujumuishaji wa huduma za kifedha kidijitali nchini.
“Mchezo wa Mpira wa miguu ni kitu ambacho kinachowaunganisha watanzania wengi na dunia nzima kwa ujumla. Kupitia kampeni hii tunataka wateja wetu wafurahie mapenzi yao ya soka huku wakinufaika na urahisi wa huduma za fedha kidijitali. Tunafurahia kuwapa wateja wetu uzoefu wa kipekee na zawadi zinazoweza kubadilisha maisha yao kupitia Mixx,” alisema Angelica Pesha.
Katika kipindi chote cha kampeni, Mixx na Hisense wataendesha shughuli mbalimbali za uhamasishaji nchini, kukabidhi zawadi kwa washindi kila wiki.
Akizungumza kwa niaba ya Hisense Bi. Tahera Karim, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Mars Communications Ltd (wauzaji na wasambazaji wa vifaa vya kieletroniki vya Kampuni ya Hisense) alisema ushirikiano huo unalenga kuwaletea Watanzania msisimko wa kusheherekea Kombe la dunia kupitia zawadi mbalimbali.
“Kombe la dunia ni moja ya matukio makubwa zaidi ya michezo duniani, na tunafurahia kushirikiana na Mixx kuwapa Watanzania nafasi ya kuwa sehemu ya uzoefu huu wa kipekee. Kupitia kampeni hii, wateja hawatajishindia zawadi pekee bali pia wataendelea kusherehekea mapenzi yao ya mpira wa miguu,” alisema Bi. Tahera
Mbali na zawadi na burudani ya soka, kampeni hiyo pia inalenga kuhamasisha Watanzania pamoja na wafanyabiashara wadogo kutumia zaidi huduma za malipo ya kidijitali kama Lipa Kwa Simu kwa miamala salama, rahisi na haraka zaidi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Bi. Angelica Pesha, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kampeni ya “Jimixx FIFA World Cup 2026 na Hisense” iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kulia ni Bi. Tahera Karim, Afisa Mkuu wa Uendeshaji - Mars Communications Limited (wauzaji na wasambazaji rasmi wa vifaa vya kielektroniki vya Kampuni ya Hisense). Kampeni hiyo ambayo imezinduliwa kwa ushirikiano na Hisense, itawawezesha wateja kujishindia zawadi za fedha taslimu za kila siku zenye thamani ya Sh milioni 1, vifaa vya majumbani ikiwemo televisheni, friji na spika za PartyBox, pia kuna safari ya bure kwenda Mexico kwa washindi watano na mshindi wa jumla ambaye ataondoka na zawadi kuu ya Sh milioni 50 mwishoni mwa kampeni.




0 comentários :
Post a Comment