DKT. MWIGULU: ACHENI UBOSI KWENYE KAZI ZA WATU



WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa Serikali waache kufanya ubosi kwenye kazi za watu na pia waziheshimu kazi zao.

"Lazima tuheshimu kazi za watu, tuheshimu jitihada za kila mmoja na tusifanye ubosi kwenye kazi za watu," alisema.

Waziri Mkuu alitoa wito huo jana jioni (Jumamosi, Mei 23, 2026) wakati akizungumza na wakazi wa Iringa mjini katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Kichangani, Kihesa, nje kidogo ya Manispaa ya Iringa.

Sambamba na wito huo, Waziri Mkuu alimwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Heri James awape maelekezo watumishi waliopo kwenye Halmashauri zote za mkoa huo na kuwataka waache kukamata vitendea kazi vya wananchi.

"Mkuu wa Mkoa watangazie viongozi wa Halmashauri zote za mkoa wako wasikamate vitendea kazi vya wananchi. Sitaki kusikia sahani wala bakuli ya mama lishe imekamatwa," alisema na kuonya kuwa endapo vitendea kazi hivyo vimehusika na kazi za uhalifu kama ujambazi, ubakaji, dawa za kulevya au meno ya tembo ndipo vinaweza kuchukuliwa kama vidhibiti kwani hayo ni makosa ya jinai.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amefanikisha kurejeshwa sh. 600,000 kwa Bw. Gideon Sebastian Yona ambazo zilikuwa ni za mtaji wa biashara yake ya dagaa. Akielezea kero yake mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Yona alisema kuwa Februari 26, mwaka huu alipofika soko la Mlandege, Iringa alikuta magunia yake ya dagaa yameibiwa na akaripoti kwa mwenyekiti wa soko lakini hadi leo hajarudishiwa dagaa wala fedha yoyote.

Alipoulizwa kama analifahamu suala hilo, Mwenyekiti wa soko hilo, Kessy Michael Ndandu, alikiri kulitambua na kwamba siku hiyohiyo ya tukio alitoa taarifa kwa Afisa Biashara wa Manispaa, Bw. Mahenge Misinzo. Alisema alichukua hatua hiyo kwa sababu walinzi wa soko ni waajiriwa wa Halmashauri.

Alipoulizwa na Waziri Mkuu kama analitambua suala hilo, Afisa Biashara huyo, alidai kwamba amepata taarifa jana yake (Ijumaa, Mei 22, 2026) ndipo Waziri Mkuu alipokemea tabia ya kuzoea matatizo ya wananchi na kumuamuru yeye na wasaidizi wake wachange hiyo hela na wamlipe hapohapo sh. 600,000 zake.

Alipopewa fedha hiyo, Bw. Yona huku akiwa na tabasamu la nguvu, alirudi kumshukuru Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kumsaidia arejeshewe mtaji wake.

Waziri Mkuu alisikiliza kero mbalimbali zilizohusu ajira, ardhi, mafao, fidia na madeni ya wazabuni, ambazo baadhi alizitolea maamuzi, nyingine alizielekeza kwa mawaziri wa kisekta waliokuwepo na nyingine kwa viongozi wa Mkoa wa Iringa.

Mapema, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile alisema kuwa katika kuimarisha mawasiliano ya Kanda ya Kusini, Serikali imeidhinisha kiasi cha shilingi trilioni 3.3 kwa ajili ukarabati wa reli ya TAZARA ili kuboresha usafirishaji wa mazao na madini kutoka kwenye mikoa mbalimbali.

“Reli ya TAZARA ni ya kihistoria lakini imesuasua kwa miaka mingi. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliridhia na zimeidhinishwa dola za Marekani bilioni 1.4 sawa na shilingi trilioni 3.3 ili kufanya maboresho ya reli hiyo yenye urefu km. 1,860 kutoka Dar es Salaam hadi Zambia. Ikikamilika, itasaidia kubeba mizigo kutoka mikoa ya Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe,” alisema na kuongeza kuwa mbali na mazao ya chakula, mizigo mingine itakuwa ni ya madini, maparachichi na mahindi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba alisema mkoa wa Iringa umepokea sh. bilioni 124 ili kuhakikisha nishati ya umeme inapatikana mkoani humo. Hata hivyo, alikiri uwepo wa changamoto za wananchi waishio maeneo ya vijijini lakini wanaonekana kuwa wako maeneo ya mijini na hivyo kushindwa kumudu gharama za kuunganisha umeme.

“Nimepata taarifa kuwa mitaa ya Ugele na Mkoga ni ya pembezoni, kata zake zinaonekana ziko mjini lakini wananchi wake wanaishi kijijini na kiuhalisia hawawezi kumudu gharama ya sh. 320,000 ya kuunganisha umeme. Kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, tumewaingiza kwenye bajeti ya mwaka ujao, kwa hiyo tutawaunganishia umeme kwa sh.27,000/-,” alisema.

Naye, Mbunge wa Iringa, Fadhili Ngajilo alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa sh. bilioni 4.4 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la halmashauri ambalo kazi ya ujenzi imeshaanza.

Aliomba kupatiwa barabara za lami walau km. 50 ili kuboresha miundombinu ya mawasiliano ndani ya manispaa ya Iringa. Pia aliomba ijengwe barabara ya kutoka Iringa hadi Manyoni kupitia Pawaga ili kuwapunguza safari watu wanaosafiri kutoka mikoa ya Kusini kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa wasilazimike kuzungukia Dodoma.

About Judith Mwaheleja

I am a Tanzanian Blogger , Entrepereneur and Fashonista.

0 comentários :

Post a Comment