WANAWAKE MKIPATA PESA MSISAHAU MILA NA DESTURI ZETU" DKT GWAJIMA


Kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoani Geita kimepambwa na ujumbe mzito wa kuwataka wanawake nchini kuzingatia mila na desturi zinazojenga jamii, huku wakizidi kupiga hatua kubwa za kiuchumi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Machi 8, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema mafanikio ya kiuchumi hayapaswi kuwa chanzo cha kubomoa misingi ya familia.

Dkt. Gwajima amebainisha kuwa Serikali imekuwa ikiunda majukwaa mbalimbali kama mpango mkakati wa kuimarisha kipato cha mwanamke ili kupunguza ukatili majumbani. 

Hata hivyo, amesisitiza kuwa wanawake wanapaswa kulinda kizazi kijacho kwa kuzingatia mila bora.

"Serikali inaimarisha uchumi wa mwanamke mmoja mmoja ili kupunguza ukatili, lakini hatupaswi kusahau mila na desturi zinazojenga ili kulinda kizazi chetu," alisema Dkt. Gwajima".

Naye Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee kutoka Zanzibar, Mhe. Zawadi Amour Nassor, ametoa rai kwa wanawake kutodharau nafasi ya mwanaume ndani ya familia wakati wakidai haki zao.

Amesema kuwa pamoja na mapambano ya usawa, mwanamke hapaswi kusahau kuwa mwanaume ni kiongozi wa familia na anapaswa kupewa utii unaostahili. Aliwaasa wanawake kutokuwa chanzo cha kuvunjika kwa ndoa zao kwa kisingizio cha kusaka haki.

Katika hatua nyingine ya kihistoria, Mkoa wa Geita umezindua mradi wa mpango wa kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto ujulikanao kama PAMOJA.

Mradi wa PAMOJA unatekelezwa katika mikoa 10 na halmashauri 40 nchini, chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) kwa thamani ya dola za kimarekani milioni 104 sawa na sh bilioni 262 za kitanzania.

Mkuu wa mkoa wa Geita Martin Shigela amesisitiza kuwa mradio huo unaenda kumaliza Hali ya ukatili katika jamii ya mkoa wa Geita ambapo kupitia mradi huo wanawake na watoto watasaidika.












About Judith Mwaheleja

I am a Tanzanian Blogger , Entrepereneur and Fashonista.

0 comentários :

Post a Comment