Wednesday, 28 August 2024

JAMII YAASWA KUENDELEA KUPAZA SAUTI KUKEMEA VITENDO VYA UKATILI

NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


JAMII imeaswa kuendelea kupaza sauti zao kwa kukemea vitendo vya ukatili ambavyo vimekuwa vikiendelea kushamili katika maeneo mbalimbali kwenye jamii inayotuzunguka ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua.

"Ukisikia kuna tukio la ukatili wa kijinsia kwa mwanamke au mtoto, hebu fikiria je ingekuwa amefanyiwa mtu wako wa karibu au familia yako ungejisikiaje? hivyo kama wanaharakati wa masuala ya Jinsia tunapaswa kupaza sauti ili mamlaka zichukue hatua na kukomesha vitendo hivyo".

Hayo yamesemwa leo Agosti 28, 2024 na Mwezeshaji Clara Godson katika mwendelezo wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) zinazofanyika kila Jumatano katika ofisi za Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Mabibo jijini Dar es Salaam.

Kwa upekee wake hii leo, wana - GDSS wamefanya tathimini ya juu ya mada mbalimbali walizojifunza katika semina hizo za kila wiki ikiwa ni mkakati wa jukwaa lao ambalo linawapatia fursa ya kupaza sauti inayotoa fursa ya kuleta haki na usawa kwa jinsia zote.

Bi. Clara amewasisitiza wana-GDSS kwa kusema kuwa, tukio la ukatili wa kijinsia linaporipotiwa mahali popote pale, wao ndio wanaopaswa kuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti na kisha makundi mengine ya kijamii yaungane nao katika kupaza sauti.

Naye mmoja wadau wa Semina za Jinsia na Maendeleo, Kenedy Angeliter amesema, wanaharakati wa masuala ya jinsia kote nchini ni watu wazuri na wapenda mabadiliko wakiwa na azma ya kufikia usawa wa kijinsia, hivyo wanavyopaza sauti zao katika matukio ya ukatili wanafanya hivyo kwa lengo la kuonesha kwamba wanapinga kila aina ya unyanyasaji na kuchangia mabadiliko katika ngazi ya jamii.

Jukwaa la GDSS lililanzishwa mnamo mwaka 1996 na kwa miaka yote hiyo semina za jinsia na maendeleo hazijawahi kukosekana na zinafanyika kila Jumatano ambapo washiriki wa semina hizo wamekuwa wakinoa uelewa wao kuhusu masuala ya jinsia na maendeleo

Moja ya manufaa yaliyotokana na Semina za Jinsia na Maendeleo ni kuanzishwa kwa vituo vya taarifa na maarifa (KC) katika maeneo mbalimbali nchini ambavyo vimewezesha kuibuliwa kwa matukio ya ukatili katika jamii.










No comments:

Post a Comment