Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) unapenda kutoa ufafanuzi rasmi na kuweka mambo wazi kufuatia taarifa zisizo sahihi na zinazoleta utata zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mkutano uliofanyika hivi karibuni Ikulu.
Kusudi Halisi la Mkutano
TBN inathibitisha kuwa madai haya si sahihi na yamekuwa yakipotoshwa.
Kusudi la kweli na la moja kwa moja la wito wa Ikulu lilikuwa hili: Mkurugenzi mpya wa Mawasiliano Ikulu, Bw. Bakari Machumu, alifanya mkutano wa utambulisho rasmi na wadau muhimu wa sekta ya habari, akianza na wanahabari wa maudhui ya mtandaoni.
Mkutano huu ulikuwa ni hatua muhimu ya kuweka msingi wa ushirikiano na mawasiliano bora. Hakukuwa na ajenda iliyofichwa, wala mchezo wa nyuma ya pazia. Taarifa zozote zinazozungushwa kinyume na ukweli huu zinapaswa kuchukuliwa kama za uzushi na zisizo na msingi.
Wito wa Utulivu na Maadili
TBN inasikitishwa na kitendo cha kusambazwa kwa kipande kifupi cha video cha mkutano huo na baadhi ya watu, ikiwemo wanasiasa, kwa nia ya kujenga utata na kashfa kutoka kwenye kikao cha kawaida cha kiutendaji.
Tunasisitiza umuhimu wa kukuza utamaduni wa majadiliano ya kitaifa yenye staha na ukweli. Vitendo vya kubuni uongo na kupotosha taarifa vinadhoofisha tasnia ya habari na jitihada za kujenga uelewa katika jamii.
TBN inatoa pongezi kwa Bw. Machumu kwa kuonyesha nia ya kushirikiana na wadau wote wa habari. Tunamsihi aendelee na utendaji wake, huku tukiamini kuwa uwazi na utulivu ndio silaha bora dhidi ya upotoshaji.
Tunawaomba wananchi na wadau wote kutanguliza hekima, ukweli, na uzalendo na kukataa taarifa zozote zinazoweza kuleta mgawanyiko au kuchochea taharuki nchini.
![]() |
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bw. Bakari Machumu akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja na Waandishi wa Habari wa Mtandaoni, pamoja na Wanablogu mbalimbali, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Novemba, 2025.




0 comentários :
Post a Comment