Dar es Salaam, Agosti 21, 2025:
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi, ametaja majukumu makuu matano ambayo sekta ya habari nchini inapaswa kuyatekeleza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, akisisitiza umuhimu wa taaluma, weledi na maadili katika kuripoti.
Akizungumza kwenye Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam, Profesa Kabudi alisema vyombo vya habari ni mhimili muhimu katika kukuza demokrasia na kulinda amani wakati wa uchaguzi.
“Vyombo vya habari vinapaswa kuhakikisha wananchi wanajua haki na wajibu wao, kutoa elimu juu ya sera za wagombea, kufuatilia ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, kuhamasisha ushiriki wa makundi maalum kama vijana na wanawake, na kupambana na taarifa potofu badala ya kuzisambaza,” alisema Profesa Kabudi.
Aidha, alisisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo lazima uongozwe na misingi ya taaluma na maadili ya uandishi wa habari ili kulinda heshima ya tasnia na kuepusha vurugu au uvunjifu wa amani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Wakili Patrick Kipangula, alikumbusha waandishi wa habari kuhakikisha wanakuwa na ithibati kabla ya kufanya kazi za kihabari, hususan katika kuripoti uchaguzi.
“Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari kinasema bayana kuwa mtu yoyote anayetaka kufanya kazi ya uandishi ni lazima awe amepewa ithibati na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari. Hivyo ni kosa la jinai kwa mwandishi wa habari kufanya kazi bila ithibati,” alisema Kipangula.
Aliongeza kuwa uhalali wa waandishi wa habari katika kipindi hiki ni jambo lisiloweza kupuuzia, kwani tasnia hiyo inahusisha majukumu makubwa yanayoathiri utulivu wa taifa.
Mkutano huo uliwahusisha wadau mbalimbali wa sekta ya habari na utangazaji, ambao walijadili nafasi ya vyombo vya habari katika kulinda maadili ya kitaifa na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Mwaluko Kabudi (wa nne kutoka kushoto waliokaa), akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wadau wa sekta ya habari na utangazaji baada ya kufungua Mkutano wa Wadau wa Habari na Utangazaji Kanda ya Mashariki uliofanyika jijini Dar es Salaam. Waliokaa kutoka kulia ni Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Andrew Kisaka, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Patrick Kipangula, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Rodney Mbuya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Gerson Msigwa, pamoja na Kamishna na Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime pamoja na Mjumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Waliosimama nyuma ni viongozi wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) akiwemo Muhidin Issa Michuzi (Mdhamini), Mwenyekiti wa TBN Beda Msimbe, Mjumbe Joachim Mushi na Mweka Hazina ambaye pia ni Mtaalamu wa Habari, Cathbert Kajuna.
About Judith Mwaheleja
I am a Tanzanian Blogger , Entrepereneur and Fashonista.
0 comentários :
Post a Comment