Thursday, 31 October 2024

MKE WA RAIS ZANZIBAR AFURAHISHWA NA MCHANGO WA WAKE WA MARAIS AFRIKA


MKE wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation Mhe. Mama Mariam Mwinyi ameeleza kufurahishwa na mchango mkubwa wa wake wa Marais wa Afrika, hasa katika kutoa ufadhili wa masomo kwa fursa 2,080 kwa madaktari chipukizi kutoka nchi 52 za Afrika kwenye taaluma 44 muhimu zinazohitajika, kama vile “oncology,” utaalamu wa afya ya uzazi kwa kina mama, tiba ya kisukari, na magonjwa mengine.

Mama Mariam Mwinyi, ameyasema hayo leo tarehe 29 Oktoba 2024 alipozungumza katika Mkutano wa 11 wa “Merck Foundation Africa Asia Luminary” uliofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, uliowakutanisha wake wa Marais wa Afrika kutoka nchi 15.

Aidha Mama Mariam Mwinyi ametumia fursa hiyo kuipongeza “Merck Foundation” kwa kutimiza miaka 12 ya utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo kwa nchi za Afrika na Asia, pamoja na miaka saba tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi amepongeza jitihada za wake wa viongozi hao katika kusaidia jamii zao kwenye masuala ya elimu kwa wasichana, kukomesha ndoa za utotoni na ukeketaji (FGM), kupinga ukatili wa kijinsia, na kuwawezesha kiuchumi wanawake na wajane.

Akishiriki uzoefu wa taasisi yake ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) kwenye mkutano huo, Mama Mariam alieleza kwamba dhamira ya ZMBF tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 ni kujitolea kuimarisha ustawi wa jamii, kuboresha maisha bora kwa wote kwa lengo la kuboresha lishe na huduma bora za afya ya uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana.

Mama Mariam Mwinyi amesema ZMBF imefanikiwa kuwafikia wanajamii 17,000 kwa huduma za afya ya uzazi, huduma ya mama na mtoto, pamoja na kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza.

Aliongeza kuwa, kupitia mradi wake wa “Tumaini Kits” unaolenga afya ya uzazi, ZMBF imefikia wasichana 5,033 waliopo shuleni na kuwapatia taulo za kike kwa ajili ya hedhi salama.

Mkutano huo wa siku mbili uliwakutanisha wake wa Marais wa Afrika kutoka nchi 15, pamoja na mafunzo kwa waandishi wa habari na washirika wao, ambapo pia walijadili kuhusu matumizi ya kidijitali katika kujenga uelewa kwa jamii juu ya kutambua uhalifu wa mitandao na kukomesha vitendo vya kikatili kupitia mitandao ya kijamii.














No comments:

Post a Comment