Sunday, 4 August 2024

Benki ya NBC Yashiriki Tuzo za TFF 2023/24 Yaahidi ‘Kunogesha’ Ushindani Zaidi.


Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, Benki ya NBC jana ilishiriki kikamilifu kwenye tukio la utoaji wa tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini, TFF 2023/2024 huku ikiahahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote wa ligi tatu inazozidhamini ikiwemo Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na Ligi ya Vijana ya NBC ili kuvijengea uwezo utakaochochea ushindani zaidi miongoni mwao.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Bw Waziri Barnabas aliemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Theobald Sabi alisema benki hiyo imejipanga zaidi kuhakikisha kwamba udhamini wake kwenye ligi hizo unakuwa chachu muhimu katika kuvisaidia vilabu hivyo kuwa bora zaidi kupitia usajili wa wachezaji wenye viwango vizuri zaidi sambamba na kuboresha mabenchi yao ya ufundi.

“Leo hii kila mtu ni shahidi wa namna ambavyo tuzo hizi zimeongeza mvuto mbele ya wapenda soka wote hapa nchini kutokana na ushindani mkubwa uliopo miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwania tuzi hizi wakiwemo kutoka ndani na nje ya nchi. Ushindani huu unatokana na ubora walionao wachezaji husika ambao chimbuko lake ni usajili mzuri unaofanywa na vilabu vinavyoshiriki ligi hizi. Jukumu letu kama wadhamini wakuu wa ligi hizi ni kuhakikisha kwamba vilabu vinaendelea kuwa na nguvu hiyo zaidi,’’ alibainisha Waziri

Katika tuzi hizo ilishuhudiwa maofisa mbalimbali wa benki hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki hiyo Bw Elibariki Masuke, Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki wa benki hiyo Bw Msafiri Shayo na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki hiyo Bw Raymond David wakikabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali wa tuzo hizo.

Aidha Bw Waziri akipata heshima ya kushiriki sambamba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa kukabidhi Tuzo ya Mchezaji Bora Ligi Kuu ya NBC (MVP) kwa mchezaji Aziz Ki kutoka klabu ya Yanga SC ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia heshima hiyo ni kwa niaba ya maofisa wengine na Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Bw Theobald Sabi, Waziri alisema imekuwa ni fahari kwao kama wadhamini wakuu kupewa heshima hiyo hali iliyothibitisha thamani ya mrejesho chanya kutoka kwa wadau wa mchezo wa mpira hapa nchini.

“Heshima hii tunayoendelea kuipata kupitia mchezo huu pendwa inatusukuma zaidi kuendelea kuwekeza nguvu zetu zaidi si tu kwenye mchezo huu bali pia michezo mingine ikiwemo riadha, golf na michezo mingine ambayo imekuwa ikitusaidia kusukuma agenda zetu mbalimbali zinazolenga kusaidia jamii hususani kwenye masuala ya afya ya mama na mtoto.’’ Aliongeza.

1

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa (wa pili kushoto) akikabidhi tuzo ya Mchezaji Bora Ligi Kuu NBC 2023/24 (MVP) kwa mchezaji Aziz Ki ( wa pili kulia) kutoka klabu ya Yanga SC ya jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya tukio la utoaji Tuzo za TFF 2023/24 iliyofanyika jijini Dar es Dar es Salaam jana. Wanaoshuhudia ni Rais wa TFF , Wallace Karia (Kulia) na Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Bw Waziri Barnabas (Kushoto). Benki ya NBC ni mdhamini Mkuu wa ligi hiyo.
2
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Bw Waziri Barnabas (Kushoto) akikabidhi tuzo ya Kocha Bora Ligi Kuu NBC 2023/24 kwa Kocha Miguel Gamondi (katikati) kutoka klabu ya Yanga SC ya jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya tukio la utoaji Tuzo za TFF 2023/24 iliyofanyika jijini Dar es Dar es Salaam jana. Benki ya NBC ni mdhamini Mkuu wa ligi hiyo.
4
Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki ya NBC Bw Elibariki Masuke (kushoto) sambamba na Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidau (Kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na Washindi Tuzo ya Seti Bora Ya Waamuzi Ligi Kuu Ya NBC 2023/24 wakati wa hafla ya tukio la utoaji Tuzo za TFF 2023/24 iliyofanyika jijini Dar es Dar es Salaam jana. Benki ya NBC ni mdhamini Mkuu wa ligi hiyo.
5

Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki hiyo Bw Raymond David (kushoto) akikabidhi Tuzo ya Mwamuzi Bora Ligi Kuu Ya NBC Tanzania 2023/24 kwa mwamuzi Ahmed Arajiga wakati wa hafla ya tukio la utoaji Tuzo za TFF 2023/24 iliyofanyika jijini Dar es Dar es Salaam jana. Benki ya NBC ni mdhamini Mkuu wa ligi hiyo.
6
Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC Bw Waziri Barnabas (Kushoto) akibadilishana Mawazo na Rais Mstaafu wa TFF Leodgar Tenga wakati wa hafla ya tukio la utoaji Tuzo za TFF 2023/24 iliyofanyika jijini Dar es Dar es Salaam jana. Benki ya NBC ni mdhamini Mkuu wa ligi hiyo

No comments:

Post a Comment